Makamu wa Rais wa Cuba atembelea Viuadudu Kibaha
Na Gustafu Haule,Pwani
MAKAMU wa Rais wa Muungano wa nchi ya Cuba Salvador Valdes Mesa amefanya ziara ya kutembelea na kukagua kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano wa nchi mbili ikiwemo Tanzania na Cuba ambapo kazi yake ni kuzalisha viuadudu wa kutokomeza mazalia ya Mbu pamoja na kutengeneza dawa mbalimbali kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia mazao.
Kiongozi huyo mkubwa kutoka nchini Cuba amefanya ziara hiyo Januari 24 mwaka huu akiambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania akiwemo Balozi anayewakilisha Tanzania nchini Cuba Humphrey Pole pole.
Viongozi wengine waliokuwepo katika msafara huo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji ,Waziri wa afya Ummy Mwalimu,Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki wakipokelewa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.
Aidha ,akiwa katika kiwanda hicho makamu huyo wa Rais alitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho na kisha kuzungumza na viongozi mbalimbali pamoja wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Baadhi ya madaktari na wafanyakazi wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha katika ziara ya Makamu wa Rais wa nchini Cuba aliyofanya kiwanda hapo jana. Katika hotuba yake Makamu wa Rais Valdes Mesa, amesema kuwa anashukuru kwa kufanya ziara hiyo nchini Tanzania hasa katika kutembelea kiwanda hicho na kwamba historia ya nchi hizo mbili ilianza miaka mingi hususani katika maeneo ya ushirikiano ya uwekezaji.
Amesema, uanzishwaji wa kiwanda hicho umetokana na mazungumzo ya pamoja na viongozi wa juu ambapo lengo lake ni kutokomeza Malaria na kwamba kiwanda hicho ni kikubwa barani Afrika.
Amesema,Cuba itaendelea kutoa ujuzi kwa ajili ya kuendeleza kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha dawa za kutokomeza viuadudu wa Malaria na hata kuua wadudu wanaoshambulia mazao.
"Ujio wangu hapa ni mara ya pili kwani mara ya kwanza nilikuja mwaka 2016 na leo 2024 nimekuja tena, lakini yote haya tunafanya kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wetu hasa katika kuhakikisha kiwanda hiki kinazidi kuimarika,"amesema Valdes Mesa Makamu wa Rais wa Cuba.
Hatahivyo,amesema umuhimu wa kiwanda hicho ni mkubwa kwani licha ya kuzalisha viuadudu wa Malaria lakini pia ni sehemu ya kutoa ajira kwani mpaka sasa kiwanda kimetoa ajira zipatazo 100.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ,awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais , amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kufanyakazi kubwa ya kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Kunenge,amesema kazi aliyoifanya Rais Samia hapa nchini imetoa fursa kwa Mkoa wa Pwani kuwa Mkoa wa kwanza unaoongoza kwa kuwa na viwanda vingi kikiwemo kiwanda cha TBPL.
Kunenge,ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha watu kutoka nchini Cuba kuja kuwekeza Tanzania hususani Mkoa wa Pwani kwakuwa mazingira ya uwekezaji ni mazuri na Mkoa upo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.
Comments
Post a Comment