DKT.EMMANUEL NCHIMBI ATEULIWA KUWA KATIBU MKUU CCM
Na Gustaphu Haule
KAMATI kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemteua Dkt.Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho kutokana na nafasi hiyo kuwa wazi tangu Novemba 2023.
Nafasi hiyo ilikuwa wazi kutokana na aliyekuwa akishika nafasi hiyo Daniel Chongolo kujiuzulu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuchafuliwa mitandaoni.
Dkt.Emmanuel Nchimbi ameteuliwa leo Mjini Unguja katika kikao cha kawaida cha kamati hiyo iliyoketi kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha chama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Uteuzi wa Dkt .Nchimbi unakwenda kutoa taswira mpya katika kipindi hiki ambacho Taifa linakwenda kuingia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na hata ule uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Nchimbi ambaye ni nguri wa Siasa za Tanzania mpaka sasa amewahi kushika nafasi mbalimbali za kichama na Serikali ikiwemo kuwa mwenyekiti wa UVCCM,Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini kwa vipindi viwili.
Lakini pia Dkt.Nchimbi amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi,Mambo ya Ndani na Habari katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Hata hivyo,Dkt .Nchimbi ni msomi na mwenye uzoefu wa masuala ya Siasa ambapo amepata Shahada ya Uzamivu (PHD)katika Chuo cha Mzumbe kilichopo Mkoani Morogoro.
MWISHO.
💪
ReplyDelete