Chungu, tamu: Pori la Akiba la Kilombero kupandishwa hadhi

Na Monica Msomba.

 Kilombero. Ni mwendo wa saa tano kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara hadi kufika katika Pori la Akiba la Kilombero “A” lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

Nafika katika bwawa la Ndolo lililopo katika pori hilo. Nakuta hali ya bwawa hilo ni tulivu huku sehemu kubwa ikiwa imefunikwa na majani kana kwamba hakuna bwawa kabisa.

sehemu ya bwawa la Ndolo linavyoonekana katika Pori la Akiba Kilombero

Hali iliyopo sasa hivi usingeweza kuikuta miezi 10 iliyopita. Bwawa hilo liligeuka kuwa shamba la bibi kwa wavuvi na wafugaji kuvua samaki na kunyeshwa mifugo yao.

Wangeachwa waendelee kuendesha shughuli hizo ambazo ziko kinyume na sheria, huenda bwawa hilo lingetoweka kabisa na viumbe hai vilivyokuwa vikiishi katika bwawa hilo navyo vingetoweka.

Sheria ya Uhifadhi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) namba 5 ya mwaka 2009 inaeleza kuwa mtu yeyote anayekutwa katika hifadhi akifanya shughuli yoyote ya kibinadamu akikamatwa atakuwa amefanya kosa la jinai.

Kwa sasa kila kitu kimebadilika. Serikali iliingilia kati kuliokoa bwawa la Ndolo kwa kuweka utaratibu mpya wa kutoa vibali vya uvuvi na kupiga marufuku wamiliki wa mifugo kuingiza mifugo katika bwawa hilo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Pori la Akiba la Kilombero lenye ukubwa wa kilomita za mraba 6,989.3 kupandishwa hadhi kutoka Pori Tengefu la Kilombero Februari 17, 2023 kwa tangazo la serikali namba 64.

Pori hilo linalopakana na Vijiji 92 limegawanyika katika sehemu mbili ‘A’ ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,381.5 na zilizobaki ni Pori la Akiba Kilombero “B”

 Mwelekeo mpya wa uvuvi

Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Kilombero (TAWA) imeanza kutoa vibali kwa wananchi waishio jirani na pori hilo hasa wanaojishughulisha na uvuvi katika mabwawa yaliyopo ndani ya pori hilo.

Lengo la utaratibu huo ni kupambana na uvuvi haramu ili kulinda viumbe vya majini wakiwemo samaki wanaopatikana katika mabwawa la Ndolo.

Afisa Ujirani Mwema wa Pori la Akiba la Kilombero, Rehema Kaminyoge anasema wameweka miongozo ya namna ya kuvua samaki ambapo sharti mojawapo ni kusajiliwa na kupata kibali kulingana na mahitaji ya wavuvi.

Moja ya boti zinazotumika kuvulia samaki katika bwawa la Ndolo Pori la Akiba Kilombero

 Vibali vinavyotolewa ni cha miezi sita ambapo mvuvi anapaswa kulipa kiasi cha Sh15,000, kibali cha siku (Sh5,000) na kibali cha mchuuzi ambacho ni Sh 4,000. 

Pia mvuvi anatakiwa kuwa na leseni ya uvuvi kutoka halmashauri husika.

' Kasi ya wavuvi hao kukata vibali bado ni ndogo kwani mpaka Novemba 30 mwaka huu walikuwa wamekata vibali wavuvi nane lakini baada ya kuona hali hiyo kwa sasa tumeweka mpango wa kuhakikisha tunawapeleka wataalamu pale kambini ili waweze kusaidiwa kirahisi"anasema Rehema.

Wavuvi watoa ya moyoni

Mmoja wa Wavuvi katika kambi ya wavuvi ya Ishelelo, Kijiji cha Idui, Eliud Daniel (52) anaeleza furaha yake kuhusiana na mpango wa kukata vibali uliowekwa na TAWA Kilombero kwani utasaidia kulinda mazingira. Daniel ambaye ana mke na watoto watano ameishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama za kukata vibali angalau ifikie Sh.4,000 kwani viwango vilivyowekwa kwa sasa wanashindwa kumudu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Idui, John Laurent (54) anasema kuwa utaratibu uliowekwa ni mzuri na wako tayari kuutekeleza kwa kuwa shughuli ya uvuvi ndio sehemu ya kipato ambacho kinasaidia kuendesha maisha yao na hata kusomesha watoto wao.

‘’Utaratibu wa kukata vibali kwetu sisi ni mzuri kwa kuwa utasaidia wavuvi kufanya shughuli zetu tukiwa huru na hii itatusaidia kuwa na uvuvi endelevu na wenye tija ambao utatufanya tuwe na kipato cha uhakika na hivyo kuinua uchumi wa familia zetu.

“Tunaomba utaratibu wa kukata vibali uwekwe vizuri ili kuwarahisishia wavuvi kupata kibali kwa urahisi,” anasema Laurent.

 Kwa upande wake, mfanyabiashara wa samaki wa Kijiji cha Idui, Mwanaisha Katembo (43) anaiomba TAWA Kilombero kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri ambao utawasaidia wavuvi kupata vibali kwa urahisi na kuondoa usumbufu kwa wachuuzi.

Anasema kwa sasa mvuvi analazimika kusafiri umbali wa kilomita 200 kutoka katika kijiji chao mpaka kufika katika ofisi za TAWA zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa ajili ya kukata kibali.

Mwanaisha anadai jambo hilo limekuwa likiwakatisha tamaa kwa kuwa gharama ya kusafiri ni kubwa kuliko hata ile ya kukata kibali husika.

“Binafsi nimeridhishwa na utaratibu wa wavuvi kukata vibali, utaleta manufaa kwa wafanyabiashara na hata wavuvi wenyewe kwani hapo awali kulikuwa na uvuvi holela ambao ulisababisha wakati mwingine bwawa kupungua maji na hata kukosa samaki. Uvuvi huo ulikuwa unaua mazalia ya samaki,” anasema Mwanaisha, mchuuzi wa samaki .

Picha ni baadhi ya Wavuvi katika kambi ya wavuvi ya Ishelelo kijiji cha Idui Kilombero

Wadau waungana kulinda bwawa Ndolo

Mwekezaji wa kampuni ya Kilombero Safari, James Bebe anasema kuwa wanashirikiana na TAWA kufanya doria usiku na mchana ili kuzidhibiti vitendo vya uharifu na shughuli nyingine za kibinadamu ndani ya hifadhi. 

Bebe anasema hali ya uvuvi kwa sasa ni nzuri kwani wavuvi wanafuata utaratibu uliowekwa.

“Kuna sehemu tumezuia wavuvi wa kiraia hawawezi kuingia hovyo lakini mkakati mkubwa uliopo ni kuongeza ulinzii zaidi ili kuhakikisha hifadhi inakuwa salama na vitendo vya kiharifu vinakomeshwa,” anasema Bebe na kuongeza 

“Kampuni yetu imeingia mkataba wa kushirikiana na TAWA kuhakikisha tunalinda na kutunza vivutio vyote vilivyopo katika hifadhi hii, ndio maana tumeongeza nguvu ya ulinzi na sasa tunalinda usiku na mchana na hata mimi mwenyewe ninashiriki ulinzi huu."

Bebe alikuwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa vitendo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Mwekezaji wa Pori la akiba Kilombero James Bebe akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni


Umuhimu wa bwawa Ndolo

Bwawa la Ndolo ni miongoni mwa mabwawa matatu yaliyopo katika Pori la Akiba la Kilombero, Mabwawa mengine ni Ngapemba na Mende.

Mabwawa hayo yamekuwa yakizalisha samaki aina ya Vitoga, Kambale na samaki maarufu duniani aina ya “Tigerfish” ambaye amekuwa kivutio kikubwa cha watalii kwa kuwa hupatikana zaidi katika bwawa Ndolo.

Pia bwawa hilo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa hasa katika mchango wake wa kupeleka maji katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere linalojengwa katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Ndolo ni bwawa ambalo linaungana na mabwawa mengine makubwa yaNgapemba na Mende kumwaga maji yake katika Mto Mnyela na Mburi.

Mkusanyiko wa maji hayo huchangia asilimia 65 katika bwawa la Julius Nyerere.

Kamanda wa Uhifadhi Pori la Akiba la Kilombero “A”, Bedui Mboto anasema TAWA imefanya kazi kurejesha uoto wa asili katika pori hilo ambao uliharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Pia wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira hususani katika pori hilo sambamba na kuhamasishawananchi kuwa na miradi rafiki kwa uhifadhi.


Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhifadhi wa Pori la Akiba Kilombero  Bedui  Mboto {mbele kushoto}

Hatua zaidi kulinda Pori la Akiba la Kilombero

Kamanda wa Uhifadhi TAWA Wilaya ya Kilombero, Bigilamungu Kagoma anasema kwa sasa ulinzi wa pori hilo umeimarishwa na kwamba vitendo vya uharifu ikiwemo ujangili na uvuvi haramu vimepungua.

Kagoma anasema wanatumia boti maalum za doria katika mabwawa, kamera za kuchukua picha bila rubani (drone) pamoja na askari wanaozunguka katika pori hilo usiku na mchana wakiwa na silaha za moto .

Mbali na kuimarisha ulinzi lakini TAWA Kilombero tayari wameanza utaratibu wa kuweka vigingi katika maeneo ya mipaka ya pori hilo ili kuzuia uvamizi ya makazi na shughuli za kilimo.

Mpaka kufikia Novemba 2023, tayari wameweka vigingi 287 kati ya vigingi 389 wanavyolenga kuweka awamu ya kwanza.

Kagoma anasema wanatarajia kuongeza watumishi kutoka 27 mpaka 82 pamoja na vitendea kazi mbalimbali, kama vile boti huku akisema wamejipanga vizuri katika kufanya doria muda wote katika pori hilo.

Kwa mujibu wa TAWA Kilombero, katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2023, watuhumiwa 188 walikamatwa katika pori hilo kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulishaji wa mifugo hifadhini, kilimo, uvuvi haramu na ukataji wa miti kwa matumizi mbalimbali.

Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kukiuka Sheria ya Uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009, huku ng’ombe 5,109, nyavu/kokoro 35, majembe ya kukokotwa na ng'ombe 16 na matrekta matano navyo vikikamatwa.






Club News Editor; Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA