ADUI ALIYEBADILIKA: WANAKIJIJI WANAVYOPAMBANA KUTOKOMEZA UJANGILI MOROGORO


Na Julieth Mkireri,KILOMBERO

UKIWA unaingia katika Kijiji cha Idui Kilomita 200 kutoka mji wa
Ifakara miongoni mwa alama za kukutambulisha kama umefika ni vigingi vilivyojengwa kwa saruji vikiwa na urefu wa futi nne na nusu vinayoonekana juu ardhi.

Vigingi hivyo, vilivyowekwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA), ni mpaka kati ya Pori la Akiba la Kilombero na kijiji hicho kilichopo wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. 
Alama za vigingi hivyo zimewekwa ili kudhibiti wananchi wasiingie tena ndani ya pori hilo kufanya shughuli za kibinadamu kama ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita.


Kamanda wa uhifadhi pori la akiba Kilombearo ‘A’ Bedui Mboto (kulia) akitoa maelezo kwenye moja ya vigingi vinavyowekwa kwenye mipaka ya hifadhi. (Picha na Julieth Mkireri)

Kijiji cha Idui ni kati ya vijiji 92 vinavyopakana na Pori la akiba Kilombero lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 6,989.3 ambalo ni  la nne kwa ukubwa wa kilometa za mraba hapa Tanzania.

Katika kijiji hiki asilimia 90 ya wakazi wake wametoka ndani ya pori la akiba la Kilombero baada ya Serikali kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya pori hilo.

Wananchi wa kijiji hicho ambao wanajishughulisha na uvuvi na ufugaji walihamia katika kambi ya Isherero ambayo ilikuwa imetawaliwa na wafugaji.

Baada ya kuhamia katika kijiji hicho wafugaji waliondoka na kuacha wananchi waliotoka ndani ya pori la Kilombero wengi wao wakiwa wavuvi kuanza maisha mapya.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Idui John Laurent anaeleza kabla ya kutolewa watu wengi walivua bila vibali, walijenga makazi ya kudumu na kukata miti jambo lililotishia uhai wa pori hilo muhimu nchini.
 
 “Hakuna utaratibu ambao hauumizi, awali tuliitupia lawama Serikali lakini kwa sasa tunaona namna ilivyotuisaidia kila mvuvi ataingia kwa kibali na atazingatia taratibu za uvuvi pori haliwezi tena kuwa eneo la malisho,” anafafanua Laurent.

Awali mifugo hiyo, alisema, ilikuwa inachangia ukame na kuua mazalia ya samaki, wafugaji walikuwa wanaipitisha kwenye hifadhi kwa ajili ya malisho na kuingia kwenye Mto Ngapemba wakiutumia kama josho lao na sehemu ya kunyweshea mifugo.

Ili waendelee kuvua samaki wengi wamejipanga kushirikiana na  TAWA kudhibiti uvuvi haramu na mifugo inayoingizwa kinyemela katika pori hilo ambayo inaenda kuharibu uhifadhi na viumbe hai.

“Wanapozunguka na  boti wachukue angalau wavuvi wachache ambao wataonyesha maeneo yenye wavuvi haramu na sisi tuko tayari kufanya hivyo, kwani kuna uvuvi wa kuweka sumu, nyavu maarufu kama pumunda ambazo zinachangia kuua mazalia ya samaki,” anaeleza.

Anaishauri TAWA kutoa ushirikiano wa haraka pindi wanapopewa taarifa kuhusiana na wanaoingia katika pori hilo kufanya shughuli za kibinadamu kinyume cha sheria.

Anna Tivadude, mkazi wa Kijiji cha Idui, anasema mabwawa yaliyopo ndani ya pori hilo la akiba ni mkombozi kwa wavuvi na kwamba utaratibu wa vibali uliowekwa kwa sasa unaenda kuwainua zaidi wavuvi.

“Naiomba Serikali iendelee kuwadhibiti wafugaji ambao awali walikuwa chanzo cha baadhi ya mabwawa kukauka na samaki kutoweka ndani ya pori hilo,” anasema.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Idui kambi ya isherero wakiwasikiliza maafisa wa TAWA (hawapo pichani) walipotembelea kijijini hapo. (Picha na Julieth Mkireri)

Wasaidia kukamata majangili 

Samson Elias, baba wa watoto watatu na mke mmoja, anasema walifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye anatumia sumu kuvua samaki kwenye bwawa hilo.

“Mtu huyu tulimkamata saa mbili asubuhi hadi saa tatu usiku hakukuwa na askari wala uongozi wa TAWA waliofika kumchukua ilimlazimu mwenyekiti amuachie, jambo ambalo linatakiwa walifanyie kazi ili tufanikiwe malengo yetu,” anaeleza Samson ambaye anategemea uvuvi kuendesha maisha
yake ya kila siku.

Katibu wa kambi ya uvuvi ya Isherero Christopher Mhagama ambaye pia ni mvuvi anaomba TAWA kuhakikisha wanatoa vibali kwa wakati ili shughuli za uvuvi ziendelee.

Baba huyo wa watoto wanne, anasema jukumu la kulinda pori hilo ni ajenda yao ambayo wanaendelea nayo ili kunufaika na samaki wengi ambao watauzika kwa haraka sokoni. Wakati wavuvi na wakazi wengine wakifurahi na uhifadhi baadhi ya wafugaji walioondolewa katika pori hilo wanasema bado wanatanga tanga na hawajui mustakabali wao. 

Mmoja wa wafugaji waliotolewa ndani ya pori hilo Madare Luhemeja anasema, awali walikuwa wanatumia eneo hilo kwa ajili ya malishio na kuweka makazi lakini baadae walihamishwa
kutoka kwenye pori hilo.

Kama ilivyo kwa maeneo mengi ya Uhifadhi, wafugaji na wananchi wakitolewa wanatengewa maeneo mbadala, Luhemeja naye ameiomba Serikali kufanya hivyo kwao ili waondokane na adha wanayokumbana nayo kwa sasa.

Kamanda wa uhifadhi Pori la akiba Kilombero ’A’ Bedui Mboto anasema katika pori hilo kulikuwa na changamoto ya uwepo wa makazi na mifugo kwenye sehemu ya maji yanayoenda mto
Kilombero.

Mboto aliwaambia hayo Waandishi wa Habari walioshiriki mafunzo kwa vitendo ya kuripoti habari za Bioanuwai yaliyoratibiwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta
Africa na kufadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi Tuhifadhi Maliasili.

Kwa mujibu wa Mboto wananchi waliokuwa ndani ya pori hilo walikuwa wakiendesha shughuli za kibinadamu kinyume na sheria ya Uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009.

Hata hivyo, baada ya wananchi kutolewa, uhakiki wa mipaka unaendelea kwa kuweka vigingi ambapo tangu kazi hiyo ianze vigingi 287 kati ya 389 vinavyolengwa katika awamu ya kwanza
tayari vimewekwa.

Uwekaji wa vigingi hivyo unakwenda kuainisha mipaka kati ya vijiji na pori  na utaratibu huo utasaidia kudhibiti uingiaji holela wa wananchi ndani ya hifadhi na kufanya shughuli za
kibinadamu.

“Wakiendelea kuachiwa kuingia katika pori hili wanaweza kusababisha maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere kutotosheleza mahitaji katika kuzalisha umeme wa megawati
2,115.

Awali uwepo wa mifugo katika pori hilo ulisababisha wanyama ndani ya hifadhi kukimbia lakini pia sehemu ya mabwawa ilikauka na samaki kutoweka.

Mwitikio wa wananchi katika uhifadhi si matokeo ya bahati
mbaya. 

 Afisa Ujirani mwema wa Pori la akiba la Kilombero Rehema Kaminyoge anasema jukumu lao katika eneo hilo ni kutoa elimu sambamba na kujua mahitaji ya wavuvi.

“Maeneo yapo mengi lakini wavuvi wenyewe wanapenda kufanya shughuli zao ndani ya pori hili ambapo wanapata samaki wengi na wakubwa,” anasema.

Kupitia utaalamu na uzoefu katika kazi yake Rehema anasema uhifadhi wa mazingira uliofanyika ndani ya pori hilo ni sababu inayochangia mabwawa yaliyopo kuwa na samaki wengi na
wakubwa. 

Mikakati mingine ya TAWA kwa wavuvi hao ni kuwahamasisha wavuvi ambao wako tayari kujiunga kwenye vikundi ama vyama vyao ili waweze kusaidiwa kupitia kitengo cha ujirani mwema. 

Mbali ya wananchi na TAWA kusimamia uhifadhi, wawekezaji binafsi akiwemo Kilombero New Safari wamekuwa wakishikiriki kikamilifu kulilinda pori hilo ikiwemo kukabiliana na ujangili. 

Kampuni hiyo pamoja na kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wavuvi kuhusiana na nyavu sahihi za kuvulia na vitu ambavyo havifai katika shughuli za uvuvi pia inashughulika na
kutangaza utalii wa uvuvi wa burudani unaofanyika kwenye pori
hilo.

“Wapo baadhi ya wavuvi wanatumia sumu za miti shamba, mimea ya kupandwa, sumu za viwanda za kutibu kungu wa nyanya na wengine hizi zote zinaleta athari kwenye mito yetu na mabwawa ndani ya hifadhi ya kilombero zisipodhibitiwa mapema ni hatari,” anasema Meneja wa kampuni hiyo James
Bebe.

Pori la akiba Kilombero (Picha na Maktaba)


Club News Editor Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA