WANANCHI 183,519 KUONDOKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI KIBAHA BAADA YA MIRADI MITATU MIKUBWA YA KIMKAKATI KUANZA KUTEKELEZWA
Julieth Ngarabali , Kibaha PWANI.
Wananchi takribani 183,519 waliokuwa wakikabiliwa na adha ya ukosefu wa huduma ya maji safi kwa zaidi ya miaka 20 sasa wanatarajia kuachana na adha hiyo baada ya Serikali kutia saini na kukabidhi eneo lla utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati ya usambazaji maji yenye thamani ya zaidi ya sh.48 Bilioni huko Kibaha Mkoani Pwani.
Picha za matukio mbalimbali za utiaji saini utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati ya usambazaji maji yenye thamani ya zaidi ya sh.48 Bilioni huko Kibaha Mkoani Pwani baina ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dar esalaam (DAWASA) n.a kandarasi wawili China Civil Communication and Engineering Company ((CCCEC ) na Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company (SCECMC) .
Utiaji saini huo umefanyika katika viwanja vya Sekondari Pangani mjini Kibaha baina ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dar esalaam (DAWASA) na kampuni mbili za ujenzi China Civil Communication and Engineering Company ((CCCEC ) na Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company (SCECMC) na kushuhudiwa na Waziri wa maji Jumaa Aweso na Viongozi wengine Mkoani Pwani .
Wakizungumza mara baada ya hafla hiyo, baadhi ya wananchi wa Kata ya Pangani Mjini Kibaha wamesema kwa zaidi ya miaka 20 wamekuwa wakipata kero ya ukosefu wa maji safi jambo ambalo limekuwa likiwathiri kiuchumi ,kijamii na kiafya
"Tumekuwa tukitumia maji ya madimbwi na mabwawa yasiyo salama na kusababisha homa za matumbo apa maji ya rangi ya tope kabisa hivyo mradi huu ukikamilika utaleta faraja kwetu na pia wanafunzi watawahi masomo maana hawataamka saa tisa usiku tena "amesema Augostino Mdachi
Mdachi amesema asilimia kubwa ya wananchi walikuwa wanafuata maji umbali wa zaidi ya km sita hivyo kuathiri hata shughuli zao za Kila siku za kiuchumi.
Naye Asha Shabani amesema ukosefu wa huduma ya maji kutoka kwenye chanzo cha kuaminika imesababisha migogoro ya ndoa kwani baadhi yao wamekuwa wakiamka usiku kutafuta maji jambo ambalo lilikuwa likitafsiriwa na waume zao wanatumia mwanya huo kukutana na michepuko
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya Pangani Mariam Saidi ameshukuru kusainiwa kwa miradi hiyo mikubwa kwani athari alizokuwa akizipata ni pamoja na kushindwa kuhudhuria masomo pindi anapokuwa kwenye hedhi kutokana na changamoto hiyo ya maji.
Awali kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Kiula Kingu akitoa taarifa ya utekelezaji miradi hiyo ameitaja ni mradi wa maji ya kimkakati Kwala wenye thamani ya sh. 23.6 Bilion ambao utahudumia watu 7,901 wa maeneo ya Kwala na vitongoji vyake ,bandari kavu pamoja na viwanda vikubwa na vidogo 200.
Mhandisi Kingu ametaja mradi mwingine ni wa Pangani unaotarajiwa kuhudumia watu zaidi ya 46,000 wa Kata ya Pangani na baadhi ya majirani zao wa kata ya Tangini mjini Kibaha na una thamani ya sh. 8.9 Bilioni na wa tatu ni mradi wa Kimbiji mpaka chuo cha uhasibu ( TIA) utakaonufaisha watu 160,750 wa maeneo ya TAZARA,Ukonga hadi Gongola Mboto na utagharimu sh. 12.6 .
"Miradi hii yote itakamilika mwaka 2025 na itatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu chini ya usimamizi wa wahandisi wa ndani na utekelezaji wa miradi hii yote mitatu utasaidia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Maji Mkoani Pwani." amesema Kiula
Mbunge jimbo la Kibaha Mjini Mh. Silvestry Koka ameomba utekelezaji wa miradi hiyo ukamilike kwa wakati ili Wananchi na wagonjwa wanaopata huduma katika hospital ya rufaa ya Mkoa Pwani Tumbi hasa wajawazito na wa upasuaji waweze kuwa na uhakika wa huduma hiyo.
" Kibaha ina kata 14 kati yake mbili za Pangani na Viziwaziwa ndio zilikua na changamoto kubwa ya maji muda mrefu na kwamba sasa ujio wa mradi hii itabakia kata Moja ya Viziwaziwa ndio haina maji na kuomba wananchi wa eneo hilo nao wasogezewe " amesema Koka
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Abubakari Kunenge akitoa salamu amesema kwa sasa upatikanaji wa huduma za maji ni asilimia 86 kwa mujibu wa takwimu kutoka DAWASA na RUWASA na kwamba lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025
"Sisi wakazi wa mikoa ya Dar esalaam na Pwani tunasema maji ni sehemu ya huduma ya kijamii lakini pia ni nyenzo ya kiuchumi hasa Pwani ni Mkoa wa uwekezaji hivyo miradi hiyo mitatu ni muhimu sana mkono hapa" amesema Kunenge
Kunenge ameongeza kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo na hivyo kuomba wananchi wahakikishe miundombinu ya miradi ya maji inatunzwa vizuri na ankara za maji zilipwe vema.
Mara baada ya kushuhudia utiaji saini na.makabidhiano ya eneo la ujenzi , Waziri mwenye dhamana Mh. Jumaa Aweso amemuelekeza kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Kingu kupeleka mradi wa maji kata ya Viziwaziwa Kibaha eneo ambalo halina kabisa huduma hiyo na kutaka ifikapo Februari mwaka 2024 maji yawe yanatoka kwa wananchi eneo hilo
Aweso pia ameihakikishia chama cha .Mapinduzi CCM kuwa atafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maji yanapatikana na pia yale yote walioahidi kwenye Ilani ya chama hicho ifikapo 2025 inakamilika na chama hicho kitaenda kupata ushindi wa kishindo.
"Nakuagiza mtendaji wetu wa DAWASA huu mradi wa Pangani bora wafanye kazi kwa wakati na miradi hii ikikamilika wananchi wa Pwani wakitaka kuunganishiwa maji wasiletewe mizengwe waunganishiwe lakini na wao wanawajibu wa kulipia ankara ili miradi iwe endelevu" amesema Aweso
" Haiwezekani suala la manunguniko ya watu kulalamikia kubambikiziwa bili kila wakati itushinde na hivyo sasa tunakwenda kufunga luku kwenye huduma za maji. tukiamini itaondoa hii kero hii " amesema
Mwisho
Comments
Post a Comment