VYUO VIPYA VYA WATU WENYE ULEMAVU KUJENGWA RUVUMA, KIGOMA NA SONGWE - WAZIRI MKUU
Na Gustafu Haule,Dodoma
WAZIRI MKUU Mh. Kassim Majaliwa, amesema
Serikali imeanza ujenzi wa vyuo vitatu vipya vya ufundi stadi kwa
ajili ya watu wenye ulemavu katika Mikoa ya Ruvuma, Kigoma na Songwe ili
kusogeza huduma hii karibu na wananchi.
“Mradi huu katika mwaka wa fedha 2022/2023
ulitengewa shilingi bilioni tatu na katika mwaka 2023/2024 umetengewa shilingi
bilioni tatu nyingine. Tayari miundombinu ya madarasa, mabweni, nyumba za
watumishi na ofisi za walimu zimeanza kujengwa sambamba na karakana ambazo
hazihitaji majengo maalum,” amesema.
Ametoa kauli hiyo Desemba 2, 2023) wakati
akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye kilele cha maadhimisho ya
Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani katika ukumbi wa Halmashauri ya
Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa akielezea jitihada za
Serikali za kuimarisha ustawi wa jamii ya watu wenye ulemavu nchini, amesema Serikali
imetoa shilingi milioni 960 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni tisa kwenye shule
nane zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum katika mikoa ya Shinyanga (Shule ya
Buhangija); Njombe (Shule ya Idofi) na Arusha (Shule ya Longido). Mikoa mingine
ni Lindi (Shule ya Mtanga); Tabora (Shule ya Goweko); Singida (Shule ya
Darajani); Manyara (Shule ya Songambele) na Rukwa (Shule ya Msanzi).
“Kama mtakumbuka, fedha hizo zilitengwa kwa
ajili ya sherehe za miaka 61 ya Uhuru mnamo Desemba, 2022 lakini Mheshimiwa
Rais wetu kwa mapenzi makubwa alielekeza zikajenge miundombinu ya shule hizo.”
Akifafanua kuhusu kuimarisha upatikanaji wa
miundombinu ya elimu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kumalizia ujenzi
wa shule maalum ya Mbuye iliyoko Chato, mkoani Geita yenye “blocks” tatu
ikiwemo awali, msingi na sekondari ya chini na juu ambayo imekamilika kwa
asilimia 95 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200.
Kuhusu maboresho ya utoaji wa huduma za afya,
Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023, Serikali imetoa huduma
za afya kwa makundi maalumu kwa msamaha katika vituo vya kutolea ambapo jumla
ya wahitaji 5,225,761 walipatiwa huduma kwa msamaha wakiwemo watu wenye
ulemavu, na huduma hizo zimegharimu sh. bilioni 570.67.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza
Wizara ya Uchukuzi ihakikishe kuwa kila palipo na makutano ya reli na barabara
pawekwe taa za kuashiria au kifungio cha automatiki cha kuzuia na kuruhusu
magari ili kunusuru maisha ya Watanzania.
“Kutokana na kuwepo matukio ya ajali za mara kwa
mara zinazohusisha treni na vyombo vingine vya moto, TARURA na TANROADS
washirikiane na Shirika la Reli nchini kuhakikisha maeneo yote yenye makutano
yanaimarishwa kwa kuwekwa mifumo au alama zenye tahadhari ya kutosha kuweza
kudhibiti matukio ya namna hiyo.
Hatahivyo,Majaliwa amewataka wamiliki wa vyombo
pamoja na madereva wote wazingatie alama za barabarani kwa ukamilifu ili
kupunguza ajali za barabarani.
MWISHO.






Comments
Post a Comment