UHIFADHI POR LA AKIBA KILOMBERO UTAKAVYOLIOKOA BWAWA LA MWALIMU NYERERE


Ngiri wakiwa katika moja ya hifadhi Mkoani Morogoro

Na Julieth Mkireri, Kilombero.

WAKATI Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anapandisha hadhi pori tengefu la Kilombero na kuwa pori la akiba huenda wengi hawakujua eneo hilo ni muhimu kwa kiasi gani katika kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa umeme hapa nchini.

Pori  tengefu la Kilombero, lililoanzishwa mwaka 1952 wakati wa ukoloni, lilipandishwa hadhi kuwa pori la akiba Februari mwaka huu na Rais Samia, hatua iliyoongeza ulinzi na uhifadhi katika eneo hilo muhimu nchini. 


Pori la Akiba la Kilombero ni miongoni mwa maeneo muhimu katika uendelevu wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere kwa kuwa linachangia takriban theluthi mbili ya maji.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Mto Ruaha Mkuu unachangia asilimia 15 ya maji huku Mto Luega ukichangia asilimia 19 na asilimia 65 zilizobaki ni kutoka Mto Kilombero na vyanzo vyake vingine vya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Gissima Nyamo-Hanga elieleza Septemba mwaka huu kuwa  gridi ya Taifa ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,900 ambapo theluthi mbili ya umeme huo inazalishwa na gesi asilia na asilimia 30 inatokana na nguvu ya maji. Umeme kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere utaongeza nishati ya umeme kwenye gridi ya taifa mara mbili ya kiwango cha sasa hadi megawati zaidi ya 4,000. 

Wakati wa uzinduzi wa ujazaji maji wa bwawa hilo, Rais Samia alisema kuwa mradi huo utachangia kuleta maendeleo na kutimiza ndoto iliyokuwepo tangu kupatikana uhuru na kukamilika kwake kutasaidia kilimo cha umwagiliaji na kuimarisha na kufungua fursa za utalii katika eneo la kusini mwa Tanzania hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

    

Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere


Kilombero mtaji Bwawa la Mwalimu Nyerere

Alisema manufaa ya mradi huo wenye thamani ya sh.6.6 trilioni yatapatikana endapo tu utunzaji wa mazingira utazingatiwa katika vyanzo vya mabonde na mito inayoleta maji katika bwawa hilo.

 “Watu wa maeneo haya yanayozunguka bwawa  wanatakiwa kutunza mazingira, wananchi, wafanyabiashara na taasisi zote ambazo zinachepusha maji katika bonde la Mto Rufiji wazuiwe,” alisema Rais Samia na kuwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi yao ipasavyo ya kulilinda ipasavyo bwawa hilo.

Ili maji yatosheleze katika bwawa la Nyerere unahitajika ujazo wa lita Bilion 34 za maji ambazo zinatoka katika vyanzo vya mito tofauti ukiwemo  Mto Kilombero uliopo ndani ya Pori la Akiba Kilombero.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaeleza kuwa uhifadhi wa Pori la Akiba la Kilombero na maeneo jirani vinachangia kujaza maji kwa asilimia 65 na kuwezesha uzalishaji wa umeme wa megawati 2,115 unaotarajiwa kutoka katika bwawa hilo.

Pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 6,989.3  lipo katika Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Mlimba na  Kilombero mkoa wa Morogoro. 

  • "Pori hilo ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 6,989.3 limegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni Kilombero A -  yenye ukubwa wa Kilomita za mraba 2,381.5 na  Kilombero B- ukubwa wa kilomita za mraba 4,607.8."

Sehemu kubwa ya Mto Kilombero ipo ndani ya Pori la Akiba la Kilombero. 

Mbali ya kuchangia ufuaji wa umeme, pori hilo lenye bioanuai lukuki pia ni muhimu kwa utalii wa picha na uwindaji.

Kamanda wa Uhifadhi Pori la Akiba la Kilombero Bigilamungu Kagoma aliwaeleza waandishi wa habari waliotembelea ofisini kwake hivi karibuni kwamba maji katika mto huo yanatokana na mito zaidi ya 30 ikiwemo Nyame, Mpanga, Mnyera, Ndoro, Ngapemba, Kibasila na Mende ambayo maji yake yakishaungana na Mto Kilombero yanaenda katika bwawa la Mwalimu Nyerere.

Kulilinda pori hilo, Kagoma anasema baada ya kutangazwa  kuwa pori la akiba Kilombero, walianza haraka kazi ya kuhakiki mipaka ikiwa ni pamoja na kuweka alama na tayari vigingi 287 vinavyoainisha mipaka vimwekwa na kazi hiyo itaendelea kwa awamu. 

“Mipaka hii inaainishwa ili wananchi wasiingie ndani ya pori na kufanya shughuli za kibinadamu ambazo mbali ya kuathiri wanyama pia zitakuwa kikwazo cha uzalishaji wa umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linatarajiwa kuwa muarobaini wa kukatika umeme hapa nchini,” Kagoma aliwaambia wanahabari hao waliokuwepo kwenye mafunzo ya kuhifadhi Bioanuai yaliyofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.  

Kamanda wa uhifadhi pori la akiba Kilombero "A" Bedui Mboto akiwaeleza waandishi wa habari namna walivyotekeleza mradi wa kuweka mipaka katika hifadhi hiyo

Anasema mbali na kuboresha mipaka ambayo awamu ya kwanza wanatarajia kuweka vigingi 389, wanaboresha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na gari, boti kwa ajili ya kufikia maeneo yenye maji kufanya doria.

Kabla ya kuwa pori la akiba, baadhi ya watu walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo uvuvi, ufugaji na kilimo.

Wengine walijenga makazi ya kisasa kama nyumba za bati na saruji kama mijini licha ya kuwa walikuwa hifadhini.

Pori la akiba Kilombero, ambalo ni la nne kwa ukubwa Tanzania kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, limepakana na vijiji 92, hali inayofanya liwe hatarini kuvamiwa na watu wanaohaha kusaka ardhi ya kilimo na malisho.

“Kabla hatujaamriwa kutuka ndani ya hili pori wapo wafugaji walikuwa wanafuga ng’ombe na mifugo mingine ambayo ilisababisha baadhi ya wanyama kukimbia, kadhalika maji pia yalikauka na wakati mwingine sisi wavuvi tilishindwa kuvua samaki wa kutosha,” anasimulia Ally Athumani, mmoja wa wananchi waliohama kutoka pori hilo na kuanzisha kambi ya wavuvi ya Isherero katika Kijiji cha Idui wilayani Kilombero.

TAWA yazidi kukaza uzi

Kamanda  wa Uhifadhi Pori la Akiba Kilombero ‘A’, Bedui Mboto anasema baada ya taratibu za kuwatoa wananchi hao ndani ya eneo la hifadhi, wameendelea kuimarisha kudhibiti wanaoingia kwenye pori hilo kinyume cha sheria kwa kuwa wakiendelea kuachiwa wanaweza kusababisha kuathiri vyanzo vya maji na kuathiri bioanui na uzalishaji umeme.

Mbali na ufugaji na makazi, uvuvi ni moja ya shughuli muhimu ya kiuchumi katika pori hili kwa wananchi waishiio pembezoni mwa pori la Kilombero kwa kujipatia kipato na kuchangia mapato katika Wilaya ya Kilombero na Ulanga.

Hata hivyo, wengi walikuwa wakifanya uvuvi huo kiharamu kiasi cha kuhatarisha mustakabali wa pori hilo.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni bwawa lililo ndani ya pori hilo ambalo sehemu ya wavuvi walijenga makazi kiasi cha kuharibu kabisa uoto katika eneo hilo. 

Maeneo ambayo huweka makambi, wavuvi hukata miti kujengea vibanda na kuathiri uoto wa eneo hilo.

Makazi yaliyoathiri ukataji wa miti hovyo katika hifadhi ya pori la akiba Kilombero

TAWA kwa kushirikiana na halmashauri zinazozunguka pori hilo waliwapatia elimu wakazi hao ili wahame na kupisha uhifadhi katika pori kwa kuwataka waanze kukata vibali kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uvuvi. 

Wavuvi haramu wageuka walinzi

Baadhi ya wakazi waliokuwa wanafanya shughuli zao ndani ya pori hilo wanasema awali walikuwa hawaelewi madhara ya walichokuwa wanfanya ila kwa sasa wamegeuka walinzi wa kulinda maliasili hizo. 

Fadhila Sanga Mkazi wa kambi ya Isherero Kijiji cha Idui anasema hatua iliyochukuliwa na TAWA kuwatoa ndani ya pori hilo inakwenda kuleta mabadiliko kwenye uvuvi kwani awali wavuvi walikuwa hawapati samaki wa kutosha kutokana na wengine kutumia njia za uvuvi zisizo halali.

“Kuna wakati ndugu zangu wanarejea nyumbani na samaki wachache huku wakilalamika kwamba wapo walioingia usiku na kuvua na zana ambazo hazitakiwi hao walisababisha samaki kutoweka, lakini utaratibu wa vibali sasa utaenda kuleta mabadiliko na kuinua uchumi wa wavuvi,” anasema.

Katibu wa kambi ya wavuvi ya Isherero iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Christopher Mhagama anasema baada ya kutolewa ndani ya kambi hiyo wapo waliokuwa wakiingia tena kuvua samaki bila vibali lakini kutokana na ushirikiano waliokubaliana kulinda pori hilo, walifanikiwa kuwakamata.

Mhagama anasema kwa sasa baada ya vibali kuanza kutolewa hakuna malalamiko ya uvuvi haramu katika pori hili kwani kila mmoja amekuwa mlinzi wa mwingine.

Wananchi katika kambi ya Isherero wako zaidi ya 100 wakiwemo wanawake na wamekuwa wakitegemea uvuvi kuendesha maisha yao na baada ya kutolewa katika hifadhi ya Pori la Akiba  Kilombero wanafanya uvuvi wao kwa kuwa na vibali maalumu.

Tayari vibali  vya uvuvi vimeanza kutolewa kwa waishio pembezoni mwa Pori  ili kukuza vipato vyao sambamba na kujenga mahusiano kati ya wananchi na wahifadhi.

Kamanda  wa Uhifadhi Pori la Akiba Kilombero ‘A’, Bedui Mboto anaeleza baada ya kuanza kutoa leseni za uvuvi  wameanza kukomesha uvuvi haram.  Kwa sasa, wavuvi wataenda kunufaika na samaki wengi kutoka ndani ya hifadhi ya pori hilo tofauti na ilivyokuwa awali ambapo baadhi walikuwa wanatumia zana haramu za uvuvi zinazoua mazalia ya samaki.

“Huku pia tuna biashara ya uwindaji wa kitalii, watu wanakuja tunapata kipato kupitia, kupitia vyanzo vya maji vilivyopo ambavyo vinavutia ,tunao utalii wa uvuvi wa kujifurahisha (sport fish),” alisema Mboto wakati wa mafunzo hayo kwa vitendo yaliyoratibiwa na Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa na kufadhiliwa na mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Uhifadhi unakuza utalii

Chati ikionyesha mapori makubwa kumi ya akiba Tanzania

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanahabari namna ya kuripori habari za utalii, mazingira, wanyamapori na maliasili. 

Utunzaji wa pori hilo la akiba umesaidia kuimarika haraka kwa bioanuai kiasi cha kuvutia zaidi watalii huku Kagoma akieleza kuwa wageni wengi wanatoka Afrika Kusini, Marekani, Sweden, Uingereza na Ufaransa. 

Idadi ya wageni hao wa nje imeongezeka mara 80 ndani ya miaka miwili kutoka sifuri mwaka 2021 hadi kufikia 80 kati ya Januari na Novemba mwaka huu. 

“Tunayo maji ambayo yanawezesha utalii wa boti, wageni wanatembea na boti mandhari yakiwa mazuri yaliyohifadhiwa vizuri, kama ni kilimo kikipangiliwa na  chenyewe kinaweza kikawa chanzo cha utalii ambacho hakiendi kinyume na uhifadhi yote hayo tunajaribu kuyaweka vizuri,” alisema. 

Kwa mujibu wa TAWA uwindaji unaoruhusiwa katika pori hilo ni ule unaofuata taratibu za kitalii kwa kutumia kampuni za uwindaji na kwamba sio kila mtu anaruhusiwa kuwinda ili kuwa na uhifadhi endelevu.




Club News Editor, Julieth Ngarabali

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA