KIBAHA YAZINDUA PROGRAM YA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO
Julieth Ngarabali, Kibaha
Halmashauri ya Wilaya
ya Kibaha imezindua program Jumuishi ya Taifa ya malezi ,makuzi na maendeleo ya
awali ya Mtoto ( PJT MMMAM) kwa lengo la kukabiliana
na tatizo la udumavu, kuwapa huduma bora za malezi ya awali na programu za
elimu ambazo zitawawezesha watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8 kukua na
kufikia ukuaji timilifu na hatimaye kuwa watu wazima wenye uwezo wa kufanya
kazi za uzalishaji mali kwa tija hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania
pamoja na kujenga jamii yenye amani na utulivu.
Uzinduzi huo umefanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo taasisi ya Anjita Child Development Foundation,viongozi wa dini, kisiasa,sekta binafsi, wataalam mbali mbali na wamiliki wa vituo vya kulelea watoto wadogo katika halmashauri hiyo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo kaimu Mkurugenzi halmashauri ya Kibaha ,Fatuma Kisalazo amesema programu hiyo pia itasaidia kumkuza mtoto kimwili ,kiakili, lugha, kijamii, kiutamaduni, kihisia na kimaadili.
Kisalazo amewaeleza wadau hao kuwa programu hiyo inalenga kutoa huduma za afya
, lishe, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama wa
watoto wenye umri wa miaka 0 -8 na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa sekta
mbalimbali katika huduma za program hiyo.
“naikumbusha jamii kuwa jukumu la kulea watoto na kuwalinda ni la jamii nzima wazazi walezi, serikali na wadau wote kila mmoja katika eneo lake ana wajibu wa kumlinda mtoto na kadhia za aina zote’’ amesema Kisalazo.
Ikumbukwe kwamba Program hii pia itasaidia kuboresha uratibu wa huduma kwa
kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera zinazohusu masuala ya MMMAM ikiwa ni
pamoja na sheria ya Mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka
2014, sera ya afya ya mwaka 2007 ili kushughulikiwa kikamilifu mahitaji yote ya
maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8.
Afisa ustawi wa jamii ,Yahya Mbogolume amewataka wazazi kutimiza majukum yao ya kimalezi sambamba na kushiriana na walimu kufuatilia maendeleo ya watoto wanapokua mashuleni.
Wadau walioshiriki uzinduzi huo wamesema programu hiyo ni nzuri ikitekelezwa
kwa ufasaha kwani itasaidia taifa kuwa na viongozi wenye utilimifu na kuishauri
serikali kukaa na wamiliki wa vituo na kuzungumza nao kwani wanamengi
kutoka kwa watoto wanaowalea lakini wanashindwa kuyatoa kwa kutokua na
ushahidi wa kutosha.
Mmoja wa wadau Deodan Katie amesema watoto wengi wanaharibika kutokana na vipindi vilivyo kwenye runinga havina maadili kwa watoto na kundi hilo lipewe elimu ya kujielewa na wajengewe kujiamini ili wanapokutana na changamoto waweze kuripoti.
Baadhi ya wadau wa Program Jumuishi ya Taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto -PJT MMMAM wakifatilia mada mbalimbali kuhusiana na mpango huo zilizokuwa zikitolewa kwenye uzinduzi wa program hiyo wilayani Kibaha.
Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Anjita Child Development Foundation amesisitiza wadau kufanya kazi kwa kushirikiana, kutoa taarifa za utekelezaji na kuhimiza wadau na serikali katika kutenga bajeti za shughuli za malezi ,makuzi na maendeleo ya mtoto.
Kwa mujibu wa Takwimu
za Taifa za makisio ya idadi ya watu zilizotolewa na Idara ya Takwimu Taifa,
Tanzania ina takriban watoto 16,524,201 (wavulana 8,328,142 na wasichana
8,196,056 ) wenye umri wa miaka 0-8 (ambao asilimia 30 ya watu wote)
Hii inamaanisha kuwa katika kila watu watatu,kuna mtoto mwenye umri wa miaka 0 mpaka nane na kwamba kundi hili linahitaji kuangaliwa kwa karibu na kufanyiwa uwekezaji ili waweze kuwa rasilimali bora yenye tija kwa familia na Taifa.
Comments
Post a Comment