ANUSURIKA KUUAWA MARA TATU PORI LA AKIBA KILOMBERO.
Ally Libenanga aliyewahi kunusurika kuuawa mara tatu na mamba na viboko wakati akivua samaki katika bwawa la Ndolo
Na Gustaph Haule, Kilombero
ILIKUWA Novemba 23 Saa 10:30 jioni naingia katika kambi ya wavuvi ya Isherero katika Kijiji cha Idui kilichopo jirani na pori la akiba la Kilombero lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Mkoani Morogoro.
Safari hiyo ya saa ,9 iliyoanzia katika eneo la Mikumi hadi katika Kijiji hicho ilinikutanisha na Ally Athumani Libenanga (43) aliyewahi kuwa mvuvi haramu katika bwawa la Ndolo lililopo katika pori hilo.
Libenanga, baba wa watoto wanne kwa sasa ameachana na shughuli ya uvuvi haramu baada ya kukumbwa na mikasa mbalimbali ikiwemo kushambuliwa na Kiboko na Mamba ambayo imekuwa ikitishia uhai wake.
“Uvuvi haramu ni sumu,” anasema Libenanga akiwa nje ya nyumba yake ya chumba kimoja iliyojengwa kwa kutumia miti na udongo na kisha kuezekwa na nyasi .
Pichani baadhi ya nyumba za Wavuvi katika kambi ya Isherero iliyopo jirani na pori la akiba la Kilombero
Sababu kubwa iliyochangia Libenanga ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Mahenge mkoani Morogoro kuacha uvuvi haramu ni baada ya Serikali kuwaondoa watu wote waliovamia pori hilo wakiwemo wavuvi waliokuwa wakiendesha shughuli zao kinyume cha Sheria ya Uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Serikali kulipandisha hadhi pori tengefu la Kilombero na kuwa pori la akiba la Kilombero Februari 2023 ambalo kwa sasa limegawanywa katika sehemu kuu mbili yaani pori la akiba Kilombero “A” na pori la akiba Kilombero “B”.
Lengo la kupandisha hadhi pori hilo lilikuwa ni kuokoa viumbe pori wakiwemo wanyamapori ambao walikuwa hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu.
Shughuli hizo ni pamoja na uvuvi haramu wa samaki, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, mkaa, kilimo, makazi ya watu, malisho ya mifugo na uwindaji haramu wa wanyamapori.
Pori la Akiba la Kilombero ambalo liko chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) lina mabwawa makuu matatu; Ndolo, Ngapemba na Mende ambayo humwaga maji yake katika mito ya Mnyela na Mburi ambayo ni makazi ya viumbe mbalimbali wakiwemo samaki, mamba, viboko na nyoka.
Hata hivyo, upekee wa bwawa la Ndolo ni makazi ya samaki aina ya vitoga, kambale, perege na “tigerfish” ambaye ni maarufu duniani.
Umuhimu wa mito na mabwawa yaliyopo katika pori hilo ni mkubwa kwa sababu huchangia asilimia 65 ya maji katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji mkoani Pwani.
“Hifadhi ya pori la akiba Kilombero ina umuhimu wake kwa Taifa kwani mabwawa na mito hiyo ikikauka ni wazi kuwa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere nalo litakufa,” anasema Kamanda wa Uhifadhi TAWA Wilaya ya Kilombero Bigilamungu Kagoma.
Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania ( TAWA) Kilombero zinaeleza kuwa kuanzia Julai hadi Novemba 2023, jumla ya watuhumiwa 188 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya ulishaji wa mifugo hifadhini, kilimo, uvuvi haramu na ukataji wa miti kwa matumizi mbalimbali.
Miongoni mwa vielelezo viliyokamatwa ni ng'ombe 5,109, nyavu/kokoro (35), majembe ya kukokotwa na ng'ombe (16) na matrekta matano na mitumbwi mbalimbali ya magome ya miti.
Chungu ya uvuvi haramu:
Libenanga ambaye kwa sasa anajishughulisha na kilimo anaweka bayana kuwa athari za uvuvi haramu ni kubwa kwani wakati wowote unaweza kupoteza maisha, kupata ulemavu, kupotelea gerezani na hatimaye kuacha familia ikiteseka.
Hatamani tena kufanya shughuli za uvuvi haramu kwa sababu iliyaweka maisha yake rehani zaidi ya mara tatu kwa kuvamiwa na mamba na viboko wakati akivua samaki katika bwawa la Ndolo kwa nyakati tofauti.
Mwaka 2017 akiwa katika mtumbwi katikati ya bwawa hilo alijikuta amedakwa na mamba katika mguu wake wa kulia na hivyo kujeruhiwa vibaya.
"Nilipambana na mamba kwa kumchoma na fimbo yenye ncha kali mdomoni mpaka akaniachia lakini kiukweli hali yangu ilikuwa mbaya kwani aliniachia majeraha ambayo niliyauguza wa muda mrefu,” anasema Libenanga huku akionyesha sehemu ya mguu wake aliyojeruhiwa.
Haikuishia hapo, siku moja mwaka 2019 wakati anaendelea na shughuli zake za uvuvi ghafla akang'atwa na mamba katika mkono wake wa kushoto na katika purukushani akajikuta amechanwa sehemu ya kidole gumba.
Mwaka 2020 akiwa anavua samaki kwa kutumia ndoano ya mkono katika bwawa hilo alijikuta anarukiwa na mamba lakini hakuweza kuguswa kwa kuwa alikimbia, Maisha ya uvuvi haramu kwa Libenanga hayakuwa rahisi. mwaka 2022, akiwa na mwenzake katikati ya bwawa hilo walivamiwa na kiboko na mtumbwi wao wa mbao ulipinduliwa na mnyama huyo.
"Kwa sasa umewekwa utaratibu maalum wa mtu kuvua samaki katika bwawa hili na yule ambaye atashindwa kufuata utaratibu haruhusiwi kuvua samaki hapa na akikutwa askari watamkamata," anasema Rehema wakati nilipofanya naye mahojiano baada ya mafunzo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Comments
Post a Comment