WATU WATANO WAFA MAJI AJALINI MAFIA MKOA WA PWANI
Na. Julieth Ngarabali. Pwani.
Watu watano wamefariki Dunia kwa kuzama majini na wengine wawili hawajulikani walipo baada ya boti waliokua wanasafiria kwa shughuli za uvuvi Wilayani Mafia Mkoani Pwani kugonga kingo za mto Rufiji na kupinduka baharini Wilayani humo.
Boti hiyo ilikua imebeba watu 15 wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi kutoka Mafia kwenda Kibiti ambapo kati yao nane tayari wameokolewa wazima.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mh. Zephania Sumaye akizungumza kwa njia ya simu Leo Jumatano Novemba mosi amesema boti hiyo ya uvuvi ilianza safari juzi mchana ikitoka eneo la Kimbugi Mafia kuelekea eneo la Bwera Kibiti ikiwa na watu 15 ambao wanaume ni 12 na wanawake watatu wote wanajishughulisha na shughuli za uvuvi.
"Ilipata ajali katika kingo za mto Rufiji baada ya boti hiyo kujigonga katika kuta za mto Rufiji Jana mchana, kwa hiyo sisi saa nane mchana tulipata taarifa hizi na kwa sababu tulikua tumeshajiandaa kutokana na tahadhari iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa timu ya uokozi ilikua tayari tuliweza kukimbia eneo la tukio kuanza uokozi" amesema Sumaye
Aidha kati ya miili iliyopatikana ya hao watano waliokufa maji mwanamke ni mmoja na ametambuliwa kwa jina la Mwanahamisi Hamisi anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 28 mkazi wa Bungu Kibiti na wengine bado hawajajulikana majina yao.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mafia amewasisitiza Wananchi na wote wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Wilayani Mafia kuwa makini kipindi hiki cha siku tatu ambapo mamlaka ya hali ya hewa imeshatoa tahadhari ya kuwepo mvua kubwa na upepo mkali , wasitishe shughuli za uvuvi na shughuli zote za kiuchumi zinazofayika baharini adi siku hizo zipite.
Kwa mujibu wa shirika la afya Duniani WHO ni kwamba watu watano nukta moja kati ya watu laki Moja wanakufa kwa mwaka kwa kuzama maji na kwamba wengi wao ni jamii ya wavuvi katika ziwa Victoria nchini Tanzania.Takwimu hiyo zimetolewa hivi karibuni na Mratibu wa Mtandao wa kitaifa wa kuzuia kuzama kwa Maji (NDPN) kupitia Mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria. Mary Francis alipokua akizungumza na wanachama wa taasisi ya Waandishi wa habari wa kuendeleza shughuli za Bahari na Uvuvi Tanzania (TMFD) na kusema takwimu hizo ni kwa mujibu wa shirika la afya Duniani WHO.
Mwisho
Comments
Post a Comment