VIFO VITOKANAVYO NA MATATIZO YA UZAZI VIMEPUNGUA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA PWANI

 



Na. Julieth Ngarabali,  Pwani.

 

Vifo vya wajawazito  vitokanavyo  na matatizo  ya uzazi  vimepungua kutoka  vitano kwa mwaka 2021 hadi vitatu kwa mwaka huu 2023 katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi na kwamba lengo ni kutokuwa na kifo kwa kipindi kijacho.

 

Takwimu hizo ni za hospitalini  humo  ambapo  imeelezwa ni sehemu ya mafanikio ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau ya kupunguza kabisa ama kufuta vifo vya wazazi vitokanavyo na matatizo ya uzazi.

 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mbio za Coast City Marathon zilizofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mh. Abubakari Kunenge amesema Serikali imekuwa ikipambana na vifo vya mama na mtoto na changamoto zilizopo ambapo Wizara ya afya imeendelea kupambana nazo kuhakikisha zinaisha na huduma zinaboreshwa .

                                                   

Coast City Marathon na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ikishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, na Wadau mbalimbali  imeandaa mbio hizo lengo likiwa ni kutafuta fedha Kiasi cha Shilingi Milioni 240 kwa ajili ya Ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi kwenye hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi. Hospitali ya Tumbi inapokea wajawazito 2,400 kwa mwaka sawa na 200 kwa mwezi idadi ambayo imeelezwa ni kubwa inahitaji miundombinu na vifaa vya kutosha kwani iliyopo inalemewa.

 


Washiriki wa mbio za Coast City Marathon zenye lengo la kusaka sh. 240 million za ujenzi wa jengo la  wodi ya wazazi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi  wakiwa katika mazoezi mbalimbali mjini Kibaha Mkoani Pwani.


Awali Mganga mkuu wa hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Dk. Amani Malima amesema mbio hizo ni kampeni ya kukusanya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi na serikali.

 

"Ni kweli jengo la wodi  ya wazazi kwa sasa limeelemewa na wagonjwa na kulazimika kuomba msaada wa jengo lingine ambalo linasaidia kuhudumia wangonjwa wengi kwa wakati mmoja na kwamba ili kujenga jengo jipya  sh. 240 Milioni kinahitaji na ndio maana wameamua kuzitafuta kupitia mbio hizo".

 

 

Muonekano wa baadhi ya Majengo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani,  Tumbi. 

Dk. Malima amesema hospitali ya Tumbi kwa sasa inapokea wagonjwa 500 kwa siku na 2,081 kwa mwezi  na wanatoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa huo.

 

Aidha ameongeza kuwa Tumbi sasa inatoa huduma bora za  matibabu zikiwemo za kuchuja figo, vipimo vya CT- Scan na inatoa ujuzi kwa wataalam wa afya na wajawazito mara kwa mara ili kuondoa kabisa vifo vitokanavyo na uzazi

 

Amesema  hospitali ya Rufaa ya Tumbi ilipewa hadhi ya kuwa rufaa mwaka 2011  na inahudumia wagonjwa kutoka wilaya sita za mkoa huo na mikoa jirani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.

 

" Lakini pia jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, serikali inaendelea kushirikisha wadau mbalimbali ili kuchangia ujenzi wa miundombinu na vifaa tiba,” amesema.

 

Naye Mratibu wa mbio hizo za Coast City Marathon Dk. Frank Muhamba amesema wameanzisha kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ambapo katika harambee  hiyo taasisi na mashirika mbalimbali zimeshiriki  michango ya fedha na vifaa vya ujenzi

 


Baadhi ya washiriki wakiwa katika mbio za Coast City Marathon Kibaha.


Katika siku ya  kwanza ya ufunguzi mbio hizo zaidi ya sh 10 milioni  zimepatikana kwenye mbio za Coast City Marathon kati yake sh. 5 Milioni imeahidiwa kutolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

 

Msanii wa kizazi kimpya maarufu Maarifa  (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Abubakari Kunenge wakati wa uzinduzi wa mbio za Coast City Marathon mjini Kibaha zenye lengo la kutafutia fedha za ujenzi wa wodi ya wazazi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.     Picha   Julieth Ngarabali


Baadhii ya wakina mama mjini Kibaha wamesema  huduma kwenye wodi ya wazazi imeboreshwa kwani kuanzia Novemba 09  wajawazito wameanza  kupata maji ya moto  wodini .

 

" Tunashukuru namna Serikalini inavyotukumbuka wajawazito maana jumanne nilienda kumuona jirani yangu Gwantwa aliyejifungua akatuambia wanajikanda weyewe  pale pale wodini maji ya moto  yanatoka ,nilifurahi kwa kweli maana inatuvutia kupenda kuoga na kua wasafi mda wote  kwa kweli"amesema Ester Mori

 

Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA