HOSPITALI YA RUFAA TUMBI YATOA HUDUMA YA MACHO BURE
Na Gustafu Haule, Pwani
Hospitali ya Rufa ya Mkoa wa Pwani Tumbi iliyopo Kibaha Mkoani Pwani kwa kushirikiana na taasisi ya Qatar Charity imetoa huduma ya upimaji na upasuaji wa macho bure Kwa wananchi zaidi ya 1000 waishio katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Huduma hiyo ilianza kutolewa Novemba 15 mwaka huu na kumalizika Novemba 18 ambapo katika huduma hiyo wananchi walipimwa macho na yeyote aliyebainika kuwa na tatizo alipata dawa na wengine kufanyiwa upasuaji bure .
Daktari Bingwa wa Macho katika hospitali hiyo Dr.Mathew Yinza, amesema kuwa toka wameanza kutoa huduma hiyo Novemba 15 imekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kwani mpaka Sasa zaidi ya wananchi 1000 wamejitokeza na kupata huduma.
Dr. Nyinza, amesema kuwa mwananchi anayepimwa na kugundulika na ugonjwa wa macho anapata huduma kulingana na hali yake jinsi ilivyo kwani wapo ambao wanapata miwani, dawa na wengine hufanyiwa upasuaji huku akisema huduma zote zinatolewa bure.
"Hospitali yetu ya Rufaa hapa Tumbi kitengo cha macho tumeona tuwasaidie wananchi kwa kuwapa huduma bure ya upimaji macho ambayo tumeanza Novemba 15 mwezi huu lakini mpaka sasa muamko ni mkubwa kwani idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza na huduma wamepata bure,"amesema Dr.Nyinza.
Nyinza, ameongeza kuwa mpaka kufikia Novemba 17 jumla ya wananchi 40 wamefanyiwa upasuaji bure na kwamba hata hivyo katika upimaji huo matatizo makubwa yaliyogundulika ni Mtoto wa Jicho pamoja na uoni hafifu.
Kwa upande wake Mratibu wa macho Mkoa wa Pwani Dr.Eligreater Mnzava, amesema kuwa wameamua kutoa huduma hiyo hospitalini hapo baada ya kuona tatizo la macho linazidi kuwa kubwa katika jamii.
Mnzava , amesema kuwa waliamua kuweka kambi ya siku nne katika hospitali ya Rufaa Tumbi kwakuwa ipo katikati na ipo katika barabara kubwa ya Morogoro ambapo uhitaji wa huduma hiyo ni kubwa.
Aidha, Mnzava amesema huduma hizo zinatolewa bure chini ya ufadhili wa taasisi ya Qatar Charity ambayo imekubali kushirikiana na hospitali ya Tumbi katika utoaji wa huduma hiyo ambayo itakuwa endelevu katika maeneo mengine ya mkoa wa Pwani.
"Nichukue nafasi hii kuwashukuru wenzetu wa Qatar Charity kwa kukubali kushirikiana nasi kutoa huduma hii ya macho hapa hospitalini kwetu Tumbi kwahiyo niwaombe wananchi wajitokeze Kwa wingi kutumia fursa hii Kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa macho,"amesema Mnzava.
Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hiyo akiwemo Hawa Mruma , ameishukuru hospitali ya Rufaa ya Tumbi pamoja na wafadhili wao Kwa kutoa huduma hizo bure kwani imekuwa na msaada mkubwa kwao.
Mruma, amewaomba wafadhili wengine kuendelea kujitokeza kwakuwa mahitaji ya wananchi bado ni makubwa hasa katika matatizo ya kiafya ambapo amesema kuwa katika huduma hiyo amepata miwani na dawa bure.
Nae Abdallah Juma, amesema kuwa amekuwa akisumbuliwa na macho miaka mingi lakini hakujua tatizo lakini baada ya hospitali ya Tumbi kutoa huduma ya upimaji bure kumemfanya kujua tatizo la macho yake na hivyo kupata huduma ya miwani na dawa ambapo ameushukuru uongozi wa hospitali ya Tumbi kwa kutoa huduma hiyo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment