TANROAD PWANI YACHUKUA TAHADHARI KUKABILIANA NA MVUA ZA ELNINO

 




Na. Julieth Ngarabali . Pwani.

Wakala wa barabara Mkoani Pwani  (TANROAD ) katika kukabiliana na mvua za Elnino zilizotabiriwa kunyesha Oktoba  imefanya matengenezo ya kinga katika barabara zake kuu zote,  kazi inayohusisha kufukua maeneo ya madaraja kwenye sehemu za kuingilia na kutokea maji na kufukua makalvati katika barabara ya Kibaha /Chalinze Morogoro, /Segera mpaka Manga na ya Kilwa road kwa maana ya Kongowe hadi Malendego.

 

Meneja wa TANROAD Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage amesema kazi hiyo inafanyika baada ya kupata maelekezo ya Serikali kuhusu kuchukua tahadhari ya mvua za elnino .

 

Amesema walianza kwanza  kufanya ukaguzi wa madaraja yake yote 318 na makalvati 1,540  ya Mkoani wa Pwani kama hatua ya awali inayolenga kujua uharibifu na namna ya uhitaji wa matengenezo ulivyo na kisha ndio wakaingia kazini.

 

Mhandisi Baraka Mwambage ametoa  maekezo hayo  mara baada ya kutembelea na kukagua  maeneo hayo na kusisitiza  hatua hiyo ni ya awali tu katika kukabiliana na elnino .



 Wahandisi kutoka TANROAD wakijadiliana jambo wakati wa ukaguzi na kufanya tathmini ya matengenezo. 

Picha na Julieth Ngarabali.

 Meneja huyo ametaja  upande wa barabara ya Chalinze/Segera matengenezo kinga yamefanyika katika daraja la Chalinze Mzee, Mazizi, Mkombezi,Kimange na makalvati madogo madogo ambayo yapo eneo la Manga.

 

Ikumbukwe kwa Mkoa wa Pwani barabara korofi zaidi ni ile ya Chalinze/Segera ambapo mara nyingi huko nyuma imekua ikitokea katika daraja la Chalinze Mzee, Mazizi, Mkombezi na hivi karibu mwaka huu eneo la Kimange na maeneo ya vilimavilima jiran na eneo la Manga.

 

"Hii kitu inafanyika kuzuia kabisa uwezekano wa barabara kujifunga katika mwaka huu wa fedha na napenda kuwajulisha Wananchi hatua hizi tunazochukua sasa tunaita hatua kinga, ni hatua muhimu sana za awali ili kuzuia kabisa uwezekano wa maji kupita juu ya barabara na kumomonyoa kingo zake na hivyo kusababisha eneo kujifunga" amesema Meneja TANROAD Pwani.


Wakala wa barabara Mkoani Pwani  (TANROAD ) ikiendelea kufanya matengenezo kinga katika barabara zake yanayohusisha kufukua maeneo ya madaraja kwenye sehemu za kuingilia na kutokea maji pamoja na kufukua makalvati katika barabara kuu zake za Kibaha /Morogoro/Chalinze/Segera/Manga na ya Kilwa road kuanzia eneo la Kongowe hadi Malendego. Picha na Julieth Ngarabali


 

Mhandisi Mwambage ameongeza kuwa daraja la mto Ngerengere kazi hiyo ya matengenezo kinga pia imekamilika baada ya kufukua kipende cha mita 100 sehemu maji yanapotokea na Mita 60 upande mwingine na kwamba pia imefanyika daraja la Mdaula, Msufini na Picha ya Ndege.

 

" na kwa upande wa barabara ya Kilwa road kwa maana ya Kongowe hadi Malendego kule sehemu inayosumbuaga sana  hua ni daraja la Mwanambaya na na daraja la mto Ruhoi kwa hiyo kwa ujumla mpaka sasa tayari madaraja 20 yote yameshafunguliwa na makalvati  yetu 1,540  yote  yameshafunguliwa" amesema na kuongeza.

 

" Sisi TANROAD Pwani tunachoenda kufanya sasa kwa kipindi chote kile ambacho mvua itakua zikinyesha tutakuwa katika maeneo hayo na mengine yote yale tukihakikisha tunaangalia madhara yanayoendelea kujitokeza iwapo yatajitokeza kila siku na kuchukua hatua stahiki kulingana na tatizo litakavyokua linajitokeza"

 

Aidha akizungumzia matengenezo kuhusu daraja la Lukigura linalounganisha Pwani na Morogoro kupitia Wilaya ya Bagamoyo na Mvomero Mhandisi huyo amesema ni uimarishaji sehemu ambayo maji hua yanadondokea na kupita eneo la daraja na kazi hiyo ipo mwishoni inatarajiwa kukamilika ndani ya siku nne hadi tano kuanzia sasa.

 

Amewataka watumiaji wa barabara wakipita eneo lolote na kuona maji yanapita juu ya barabara watoe taarifa wasivuke kwanza wasubiri mpaka pale TANROAD itakapofanya utafiti na kuona eneo ilo ni salama na kuchukua hatua stahiki.

 

"Sisi tunapenda kushukuru Uongozi wa Wizara kupitia Waziri wetu wa ujenzi Mheshimiwa Bashungwa, pia mtendaji mkuu wetu TANROAD na bila kusahau msisitizo uliotolewa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwamba maeneo yote yenye tishio la Elnino basi yaweze kufanyiwa kazi kama maandalizi ya kukabiliana na mvua hizo " ameongeza Mhandisi Mwambage

 

Katika mwaka wa fedha wa  2023/24 Sh. 18.980  Bilioni ndio zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu na madaraja Mkoani Pwani ambapo Sh. 950  milioni ni kwa ajili ya matengenezo ya madaraja 318 na makalvati 1,540  hivyo matengenezo kinga hayo yaliyofanyika ni sehemu bajeti hiyo.

 

Baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya madaraja hayo pamoja na madereva wameshukuru  hatua hiyo ya TANROAD kuchukua tahadhari kwa kufanya matengenezo hayo.




Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA