TAIFA GAS YAONGOZA UZALISHAJI WA GESI NCHINI
Na Gustafu Haule, PWANI
Kampuni ya Taifa Gas inayoshughulika na uingizaji na usambazaji wa gesi imetajwa kuwa ni kampuni ya kwanza inayoongoza kwa uzalishaji wa gesi hapa nchini iliyofikia kiwango cha tani 7,440.
Mbali na kuongoza kwa uzalishaji lakini Taifa Gas ni kampuni iliyofanya uwekezaji mkubwa wa gesi hapa nchini inayotokana na LPG (Liguidfield Petroleum Gas) ambayo haina madhara kwa mtumiaji. LPG ni bidhaa ya gesi inayotumika kama kimiminika cha Petroli kinachotokana na mafuta ghafi (Crude Oil) ambapo kupatikana kwake kunatokana na uyeyushaji katika joto kubwa.
Meneja Mkuu wa kituo cha kuhifadhia na usambazaji wa gesi ya Taifa Gas kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam Ndugu Juma Masese, amewaeleza waandishi wa habari kuwa uzalishaji huo umepanda toka mwaka 2016 hadi sasa. Masese, amezungumza na waandishi wa habari wa mazingira na uhamasishaji jamii kutumia nishati mbadala waliofanya ziara katika kituo hicho kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali ya uhifadhi na matumizi ya gesi.
Amesema kuwa, Kampuni ilianza kama Mihani gas ambayo ilikuwa chini ya nchi ya Irani na baadae kuuzwa kwa Mtanzania ambaye anamiliki kampuni hiyo kwa asilimia 100.
Amesema, Mihani ilianza mwaka 2005 na ilianza uendeshaji wake mwaka 2007 lakini awali ilikuwa ikizalisha tani 1,440 lakini toka Taifa Gas ilipoingia uzalishaji wake umepanda ambapo kwa sasa malengo ni kuhakikisha wanafika Vijiji vyote.
Masese amesema kuwa gesi inayozalishwa na Taifa Gas ni LPG ambayo ni mchanganyiko wa gesi aina ya Butane na Propane ambapo zote zimetokana na hydrocarbons.
Masese amesema Propane ina carbon chache ambayo ndio safi zaidi wakati Butane inacarbon nyingi na kwamba Taifa Gas ina Propane asilimia 40 wakati Butane ina asilimia 60 na hiyo inapelekea Taifa Gas kuwa ya pili katika Soko la Tanzania.
Amesema kuwa LPG inatumika katika matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia,(Domestic Cooking), viwandani (Industrial Heating), uzalishaji viwandani (Industrial Manufacturing), kwenye magari (Automotive ), masuala ya mwanga (Domestic lighting), na masuala ya Ndege ( Aviation).
Ndugu Masese katika kufafanua uzalishaji wa gesi hiyo ameeleza ,katika uyeyushaji wa mafuta ghafi ndipo kunapopatikana matokeo mbalimbali ikiwemo kupata Lami,Mafuta ya Dizeli,Petroli,mafuta ya Taa,Gesi na mafuta ya Ndege ambapo njia hizo zinafanya kupata gesi nzuri ya LPG ambayo inafaa kwa matumizi ya kupikia.
"Gesi yetu ipo salama na tunahifadhia katika mitungi ya aina zote kulingana na uwezo wa mtumiaji na tuna mitungi ya kilo 3,kilo 6 na 15 na mtungi wa Taifa Gas ni salama zaidi kwa kuwa ina valvu za usalama (Safety Valve)", amesema Masese.
Masese ,amewaomba Watanzania kutumia gesi ya Taifa Gas huku wakizingatia kanuni za matumizi ikiwemo kusafirisha mtungi wa gesi ukiwa umesimama,kuacha kutumia simu wakati unapikia gesi pamoja na kuchukua tahadhari ya kufungua milango na madirisha pale unapohisi harusu ya gesi.
"Matumizi ya gesi ni mazuri kwa kuwa yanasaidia kutunza mazingira yetu pamoja na kupunguza gharama za maisha lakini kuna vitu havihitajiki wakati mtu akitumia gesi kama vile simu na kufungua milango na madirisha pale unapoona viashiria vya gesi kuvuja," amesema Masese.
Kwa upande wake afisa mahusiano wa Taifa Gas Ndugu Ambwene Mwakalinga, amesema kuwa kwa sasa Taifa Gas inavituo 22 vya gesi katika Mikoa mbalimbali hapa nchini na malengo yake ni kuhakikisha huduma hiyo inafika katika ngazi ya Vijiji.
Mwakalinga, amesema bado kuna kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kutumia nishati mbadala ya gesi kwa kuwa kiwango cha matumizi ya gesi ni kidogo na Tanzania ambapo mpaka sasa asilimia 98.9 wanatumia kuni na mkaa.
Mwakalinga, ameongeza kuwa ili kufikia malengo ni lazima kukawepo na mipango endelevu ya kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala ambapo Taifa Gas imekuja mpango wa"Give Away" kutoa mitungi bure kwa Mamalishe na mpaka sasa tayari mitungi 10,000 imetolewa.
"Ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni bado ni mkubwa hususani kwa Mkoa wa Pwani na Morogoro, kwahiyo niwaombe wananchi tujiketi katika matumizi ya gesi na tuondokane na dhana ya kusema gesi inatumika sana katika Maharage,"amesema Mwakalinga
Aidha, Mwakalinga amewaomba waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri katika kuandika habari zinazoelimisha na kuhamasisha wananchi kutumia nishati mbadala ya gesi .
Kwa upande wake afisa usalama wa kituo cha Taifa Gas Albert Gungayena, amesema kuwa kazi ya kituo hicho ni kupokea gesi kutoka kwenye meli, kuhifadhi na kusambaza.
Hata hivyo, baadhi ya waandishi wa habari waliofanya ziara katika kituo hicho akiwemo Julieth Mkireri na Sanjito Msafiri kutoka Mkoa wa Pwani wameahidi kuwa mabalozi wazuri ambao watayatumia mafunzo waliyopata katika ziara hiyo kuandika habari za kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala.
MWISHO.
Comments
Post a Comment