SERIKALI MKOANI PWANI YAANZA KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA ELNINO, YAGAWA VIWANJA BURE KWA WANANCHI WAKE

 


Na Gustafu Haule, Pwani

 

SERIKALI Mkoani Pwani imeanza kuchukua hatua ya kufanya maandalizi juu ya kuwasaidia wananchi kuepukana na maafa yanayotokana na mvua  za Elmino kama ambavyo imetangazwa na mamlaka za Hali ya Hewa Nchini(TMA).

 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Mh. Abubakari Kunenge, ameanza kuchukua hatua hiyo leo Oktoba 19 katika Wilaya ya Rufiji Kijiji cha Mohoro Kata ya Mohoro  akiwa na  na timu yake ya kamati ya ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Michael Gwimile.

 

Hatua ambayo tayari imechukuliwa ni pamoja na kuwahamisha wananchi wa Mohoro waliopo kandokando ya Bahari ya Hindi na kuwapelekea eneo mpya  lenye mazingira mazuri ya kuishi hata katika nyakati za mvua.

 

 Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho Mh. Kunenge amesema kuwa Serikali imeona ianze kujipanga na kudhibiti maafa yanayotokana na mafuriko pindi mvua zinaponyesha kwa kuhakikisha Wananchi wanawekwa katika mazingira salama.

 


Mh. Kunenge, amesema kuwa wananchi hao wamepewa viwanja bure bila kulipia gharama yoyote na kwamba kila mmoja anapaswa kufanya maandalizi mapema ya kuanzisha makazi katika eneo hilo ambalo litakuwa limeondoa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea muda mrefu .

 

" Leo tumefika hapa kwa ajili ya kufanya maandalizi ya tahadhali juu ya mvua za Elmino ambazo zimekuwa zikileta maafa kwa wananchi wetu na ukizingatia Mkoa wa Pwani umezungukwa na Bahari ya Hindi ambayo imekuwa ikijaa maji wakati wa mvua na hivyo kuleta athari kwa wananch", amesema Mh.Kunenge

 


Mh. Kunenge, amesema kuwa Kata ya Mohoro imegawanyika sehemu mbili ambayo ni Mohoro Masharikai na Mohoro Kaskazini na kuna kituo cha afya ambacho mwaka 2021/2022 kilikabiliwa na changamoto ya mafuriko lakini tayari Serikali imelifanyiakazi jambo hilo.

 

Amesema, eneo walilopata limetolewa na Wakala wa Usimamizi wa Misitu na Mazingira (TFS) ambapo ndani yake kunajengwa huduma zote za jamii ikiwemo kituo cha afya,Shule,Soko , makazi na mahitahi mengine .

 



Amesema, upatikanaji wa viwanja hivyo umetokana na juhudi za Rais Mh. Dkt .Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyeridhia kugawa eneo hilo kwa wananchi wake na kwamba hakuna budi ya kumshukuru kwa hatua hiyo kubwa.

 

"Niwaombe wananchi wa Mohoro muungeni mkono Rais Samia kwa hatua hii kubwa aliyoifanya kwa kuhakikisha wote tunahamia katika maeneo tuliyopangiwa na sisi leo tumekuja kuwahamasisha ili muweze kuhama mapema," amesema Kunenge

 

Katika  hatua nyingine Kunenge , amesema mbali na hatua ya kugawa viwanja bure lakini pia tayari Serikali ipo katika mpango wa kujenga daraja jipya la Mohoro ambalo mara nyingi wakati wa mvua hujaa maji na hivyo kuleta maafa kwa wananchi na wakati mwingine kukosa mawasiliano baina ya pande mbili.

 

Amesema ujenzi wa daraja hilo tayari usanifu umefanyika na sasa imefikia hatua ya manunuzi na kwamba mkandarasi akipatikana Novemba mwaka huu daraja litaanza kujengwa.

 

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Mohoro Said Hamisi , ameishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kuwahamisha katika eneo hilo na kuwapa viwanja bure ambapo amesema wataitumia nafasi hiyo vizuri kwa ajili kujenga makazi yao ya kuishi.

 

Hamisi,amesema katika jambo kubwa ambalo Serikali imefanikiwa ni kuwatengenezea wananchi mazingira mazuri ya kuishi kwani walikuwa wanapata shida kubwa ya kupoteza ndugu zao, watoto na kupoteza mali zao wakati mafuriko yakitokea.

 

MWISHO


Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA