PWANI WAANZA KUWEKEZA KWENYE MAKUZI, MALEZI NA MAENDELEO YA AWALI YA WATOTO WA MIAKA SIFURI MPAKA NANE

 

Na. Julieth Ngarabali.mwananchi Pwani

E-Mail: jngarabali@mwananchi.co.tz

 

     
Picha za tukio la uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT -MMMAM) Mkoani Pwani.

 

Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) imezinduliwa Mkoani Pwani huku ikilenga kutoa huduma za afya, lishe, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi nane wakue kwa utimilifu na baadae kupata viongozi wenye maadili mema na tija kwa Taifa.


Pia programu hiyo inakusudia kumkuza mtoto, kimwili, kiakili, lugha, kijamii  ,kitamaduni ,kihisia  pamoja na.kimaadili  na kwamba Pwani utakua miongoni  mwa mikoa 16 inayoanza wakati huu  kuutekeleza  baada ya mingine 10 kuwa ilikwishaaza mwaka jana,  Programu hiyo ni ya miaka mitano ,2021/2022  - 2025/26  .

 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizindua program hiyo  amesema jukumu la kuwalea watoto,kuwalinda,kuwatunza na kuwaendeleza ni la kila mzazi, mlezi, Serikali na  wadau wana wajibu wa kuhakikisha wanakua na kuishi katika mazingira yaliyobora, safi na salama na wajibu wa kwanza upo mikononi mwa baba na mama.

 

Kunenge ametoa maelekezo tisa ya kuhakikisha Programu hiyo inatekelezeka na kuleta tija Mkoani humo ikiwemo kuzitaka Halmashauri zote kutenga bajeti itakayowezesha utekelezaji wa programu hiyo, walimu wa shule za msingi na Sekondari kutoa malezi yanayolenga watoto kufikia ukuaji timilifu.

 

Maagizo mengine ni katika vituo vya kutolea huduma za afya ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo vichangamshi ili watoto wanapopelekwa kupata huduma wapate maeneo ya kuchangamsha ubongo na viongozi wa Dini kutoa mafundisho yanayolenga kukuza ubongo wa watoto.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF ya mwaka 2022  inaonyesha Mkoa wa Pwani umefikia ukuaji timilifu wa watoto kwa asilimia 48.8 katika masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na asilimia 51.2  hawakuwa katika ukuaji timilifu sababu ikiwa ni kutopata huduma jumuishi zikiwemo afya, lishe, elimu,malezi yenye muitikio na ulinzi na usalama wa watoto.

 

Awali mtaalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kutoka shirika la Children in Crossfire (CIC) Davis Gisuka amesema sababu ya kuchagua uwekezaji wa watoto katika umri wa miaka sifuri hadi nane ni ndio umri pekee katika kipindi cha binadamu ambao una uwezo wa kumfundisha mtoto akakuelewa unachomfundisha.

 

"Pia  miaka sifuri adi nane ndicho kipindi ambacho makuzi ya ubongo yanaenda kwa kasi sana ndicho kipindi ambacho ujifunzaji unakua sana akili inafanya kazi kwa kiasi kikubwa sana,kwa hiyo CIC kazi kubwa tunayofanya ni mradi wa elimu na malezi kwenye eneo la umri huo"amesema Devis

 

Mwakilishi wa mtandao wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto nchini Tanzania ( TECDEN) ,  Isaack Idama ameongeza kuwa uwekezajj unaopaswa kufanyika ni pamoja na kukabiliana na tatizo la udumavu, kuwapa huduma bora za malezi ya awali na programu za elimu ambazo zitawawezesha kukua na kufikia ukuaji timilifu na hatimaye kuwa watu wazima wenye uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa tija .

 

Mkoani Pwani taasisi ya Anjita Child Development Foundation kwa kushirikiana  na Serikali ndio inatakeleza Mpango huo wa PJT MMMAM kupitia mradi wa mtoto kwanza unaoratibiwa katika ngazi ya Taifa na shirika la TECDEN .

 

Kwa mujibu wa takwimu za Taifa za makisio ya idadi ya watu zilizotolewa na idara ya takwimu Taifa, Tanzania ina takriban watoto 16,524,201 (wavulana 8,328,142 na wasichana 8,196,056 ) wenye umri wa miaka 0-8 (ambao ni asilimia 30 ya watu wote)

 

Hii inamaanisha kuwa katika kila watu watatu,kuna mtoto mwenye umri wa miaka 0 mpaka nane.

 

Kundi hili la watoto wadogo linahitaji kuangaliwa kwa karibu na kufanyiwa uwekezajj ili waweze kuwa rasilimali bora yenye tija kwa familia na Taifa .

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA