HATUA ZA KINIDHAMU KUCHUKULIWA KWA VIONGOZI WALIOSHIRIKI UTAPELI KUUZA SHAMBA LA MIFUGO KWA WANANCHI

 





Na Julieth Mkireri,  KIBAHA PWANI

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi walioshiriki kuwatapeli wananchi na kuuza maeneo katika shamba la mifugo Mitamba Kibaha.

 





Kunenge amesema wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni pamoja na mabalozi kumi, watendaji wa Serikali wawili na wenyeviti wa Serikali za mitaa watano ambao wanatuhumiwa kushirikiana na matapeli kuwauzia ardhi wananchi kinyume cha sheria.

 

Ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza na wakazi wa Mtaa wa  Lumumba kata ya Pangani alipofanya mkutano kuzungumza na wananchi hao kuhusiana na maelekezo yaliyotolewa na serikali kwa wananchi waliovamia katika kiwanja namba 34.

 

Vile vile Kunenge amemuelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kuwafanyia mahojiano watuhumiwa 24 ambao wanatuhumiwa kuhusika na uuzaji wa ardhi katika shamba hilo.

 

Kunenge pia amewataka wananchi walioendeleza maeneo yao katika kiwanja namba 34 kuondoa maendelezo yao ndani ya siku 14.

 

" Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha nakupa siku 60 anzeni kutekeleza maagizo kwa kupanga mji , baada ya hapo ambaonwatakuwa nje ya eneo la makazi watatakiwa kupisha " amesema.

 

Maagizo mengine yaliyotolewa na Mkuu huyo wa mkoa ni Mkurugenzi na wataalamu wa mji kuhakikisha wanafanyia kazi upimaji wa awali ili kuonyesha maeneo ya kiwanja namba 34 ijulikane pamoja na maeneo ya Taasisi,  kazi ambayo inatakiwa kufanyika kabla ya kuwaondosha waliovamia.

 

Shamba hilo la mifugo ambalo hekta 4000 zilikuwa zinamilikiwa na Serikali baadae hekari 2963 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya makazi  na shughuli za maendeleo lakini baadae wananchi waliendelea kufanya uvamizi katika kiwanja namba 34 kinyume na sheria.

Mwisho






Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA